“Jina langu ni Rhoda kutoka Kenya. Nataka kumpa Mungu utukufu kwa mambo mazuri aliyotenda maishani mwangu na katika familia yangu. Leo nasimama hapa kama shahidi wa nguvu za maombi na uzuri wa Mungu. Mwaka uliopita, nilituma ombi la maombi kwa God’s Heart TV na ninafuraha kuwatangazia kwamba Mungu ameyajibu maombi kwa njia kuu. Binti yangu alikuwa anasomea chuo kikuu cha Kenyatta na alikuwa ahitimu na shahada ya Masomo ya Mazingira lakini tulikuwa tunapitia changaomoto kuu ya kifedha katika kumsaidia kukamilisha masomo yake. Nilimlilia Mungu na akayajibu maombi yangu. Akatupa fedha kwa miujiza naye binti yangu akahitimu tarehe 19 mwezi wa Desemba, 2025.

“Nataka pia kuwaelezea kwamba kulikuwa na vikwazo lakini Mungu alijithibitisha kuwa yu mwaminifu. Hapo awali, jina lake halikuwa katika orodha ya watakaohitimu lakini baada ya mwezi wa kufuatilia hili; jina lake liliongezwa katika orodha ile na akapata kuhitimu na darasa lake. Namshukuru Mungu kwa uzuri na uaminifu wake. Pia ningetaka kushukuru God’s Heart TV na Ndugu Chris kwa kuwa vyombo vya maombi na faraja. Huduma hii ni baraka kwangu na familia yangu na ninawashukuru kwa maombi na msaada wenu.

“Kwa yeyote anayepitia changamoto leo na anasikia kukata tamaa. Mungu anatengeneza njia na kwa hakika atakupa jawabu la hali yako. Mwamini na uwe na imani. Kuhitimu kwa binti yangu ni ishara ya nguvu za maombi na uaminifu wa Mungu. Nashukuru na ningetaka kuwahimiza mwendelee kuomba na kumwamini Mungu. Ana uwezo na atakufanyia mema pia nawe. Asante, God’s Heart TV na Mungu aendelee kubariki huduma hii.”